Kasi ya Rais, Dk. John Magufuli, katika kufichua
ubadhirifu wa fedha katika taasisi za serikali imeshika kasi ,baada ya jana
kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli
Tanzania (RAHCO), Mhandisi Benhadard Tito.
Kusimamishwa kwa mkurugenzi huyo kumeelezwa ni kupisha
uchunguzi wa kina kutokana na ukiukwaji wa taratibu za manunuzi
uliobainika katika mchakato wa utoaji wa zabuni ya ujenzi wa reli ya kati.
Kadhalika, Rais Magufuli amevunja Bodi ya Mamlaka ya Reli
Tanzania (TRL), kutokana na kutoridhishwa na jinsi ilivyoshughulikia ripoti ya
uchunguzi wa mchakato wa ununuzi wa mabehewa ya treni.
Reli ya kati imekuwa ikilalamikiwa kwa muda mrefu
kushindwa kutoa huduma za uhakika kwa wananchi kunakosababishwa na kuharibika
mara kwa mara kwa miundombinu.
Kutokana na hali hiyo, Rais Dk. Magufuli katika kampeni
zake aliwahi kueleza kuwa atajenga reli hiyo kwa kiwango cha kisasa (Standard
Gauge).
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, alieleza kuwa
Rais Dk. Magufuli amefikia uamuzi wa kumsimamisha mkurugenzi huyo baada ya
kuitisha kikao cha wataalamu kutoka wizara na taasisi mbalimbali za serikali
ambazo zinahusika katika utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa reli ya kati kwa
kiwango cha kisasa yaani ‘Standard Gauge’.
Balozi Sefue alisema mbali na Rais Dk. Magufuli
kumsimamisha kazi mkurugenzi huyo, pia ameivunja Bodi ya RAHCO baada ya
kujiridhisha kuwa haikutekeleza ipasavyo wajibu wake katika kusimamia mchakato
wa zabuni hiyo na badala yake imeonekana kutetea kilichofanyika.
0 comments:
Post a Comment